Mchango wa Rais Sheikh Abeid Amani Karume, Katika Maendeleo ya Kiswahili: Uchambuzi wa Sera, Matamko na Mipango

Authors

  • Sauda Uba Juma Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Author
  • Ahmad Yahya Sovu Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Author
  • Editha Adolph Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Author
  • Majura Nyangaywa Lugembe Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Author
  • Njana Masanja Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Author

Keywords:

mchango, lugha ya Kiswahili, sera ya lugha, matamko ya lugha, mipango ya lugha, Rais Abeid Amani Karume

Abstract

Historia inaeleza kwamba Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizotawaliwa na wageni kwa muda mrefu. Katika utawala huo, lugha ya Kiswahili ilikebehiwa na kutwezwa hivyo kutotumika katika maeneo rasmi (BAKIZA, 2020). Lugha za Kiingereza na Kiarabu ndizo zilizopewa hadhi ya juu katika shughuli za kiserikali. Hata hivyo, mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, inasemekana kuwa lugha ya Kiswahili ilihuishwa upya na kupatiwa nafasi maalumu chini ya uongozi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mheshimiwa Sheikh Abeid Amani Karume. Pamoja na dai hilo kurudiwa mara kwa mara katika machapisho mbalimbali, halijawahi kuchunguzwa kwa kina kwa kubainisha rasmi ni sera zipi, matamko yapi na mipango ipi hasa iliyowekwa na serikali yake. Hivyo, makala hii inalenga kuchunguza mchango wa Rais Karume katika kuweka msingi wa maendeleo ya Kiswahili Zanzibar enzi za uongozi wake (1964-1972), kwa kubainisha na kuchambua kwa utaratibu sera, matamko na mipango aliyoiweka. Utafiti huu ni matokeo ya data zilizokusanywa kutoka maktabani na pia nyanjani. Mbinu za usaili na hojaji ndizo zilizotumika katika utafiti huu, na data zimechanganuliwa kwa kutumia mkabala wa kitaamuli. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Sera na Mipango ya Lugha iliyoasisiwa na Haugen mwaka (1966). Kwa ujumla, matokeo ya uchunguzi yamedhihirisha kwamba Rais Abeid Amani Karume aliweka misingi imara katika kukikuza na kukiendeleza Kiswahili Zanzibar: kwa upande wa sera, alikitangaza kuwa lugha rasmi ya ofisi, elimu na vyombo vya habari; kwa upande wa matamko, aliyageuza mahutubio yake kuwa chombo cha kujenga utaifa na uzalendo kupitia Kiswahili; na kwa upande wa mipango, alisimamia utekelezaji thabiti kupitia kampeni ya kufuta ujinga, mitihani ya walimu, uundaji wa istilahi mpya na ubadilishaji wa majina ya maeneo. Hivyo, makala inapendekeza viongozi wengine kusisitiza matumizi bora ya Kiswahili katika jamii na kuenzi mchango huo wa viongozi waandamizi na waasisi kwa vitendo. Aidha, inapendekezwa tafiti zaidi zifanyike kubaini michango ya viongozi wengine wa Zanzibar waliofuata pamoja na viongozi wa nchi nyingine kwa ujumla.

Downloads

Published

2026-11-25